Hujjatul-Islam Sayyidd Mohammad Hassan Abu Torabi Fard, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amezungumzia matukio yanayojiri katika eneo la Asia Magharibi na kubainisha kuwa, mataifa ya eneo hilo na Waislamu wako kwenye mtihani wa kusimama kidete kukabiliana na kambi ya Uistikbari, Marekani na vibaraka wao pamoja utawala wa niaba wa kambi hiyo ya Uistikbari, yaani Wazayuni katika eneo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amegusia pia maadhimisho ya Siku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inakumbusha misamiati ya "Jamhuri" na "Uislamu" ikiwa ndio kauli mbiu kuu ya Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo mamilioni ya Wairan Waislamu wenye msimamo huru walipaza sauti zao katika kila pembe ya Iran katika muda wote wa mapambano yaliyong'aa ya taifa la Iran, wakitaka: kujitawala, kuwa uhuru na Jamhuri ya Kiislamu.
Abu Torabi Fard ameongezea kwa kusema: "kwa kuzingatia hali halisi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa katika muongo wa karibuni, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesisitizia kupangwa na kuchukuliwa hatua za kurekebisha vielezo vya uchumi mkuu wa nchi, ukiwa ndio kipaumbele cha kwanza; na kupewa mwaka mpya wa 1404 Hijiria jina la 'Mwaka wa Uwekezaji kwa ajili ya Uzalishaji' kunadhihirisha ukweli kwamba kuimarisha uzalishaji, kubuni ongezeko la thamani, na kuwekeza katika sekta muhimu zaidi zenye uzalishaji hususan unaotokana na sekta binafsi ni miongoni mwa hatua muhimu zaidi za kuchukuliwa kwa ajili ya kuwa na ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa".
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amebainisha kuwa, uchambuzi wa takwimu za ukuaji wa uchumi unaonyesha kuwa, uchumi wa Iran unakabiliwa na changamoto kubwa katika kuvutia uwekezaji, kuboresha mazingira ya upatikanaji wa ajira na kuchochea mahitaji ya ndani ya nchi; hivyo inapasa kuwepo na msukumo wa kuunga mkono uzalishaji wa taifa.../
342/
Your Comment